Monday, 17 June 2013

Jeshurun's Mind: Kiswahili na Mashairi

Mausia Kwa Kila Kijana Mwanamke


Dadangu ninayeenzi, pokea zangu salamu,
Popote ulipo mwenzi, nakujali ufahamu,
Hivyo nikiwa mtunzi, ninayo kubwa hamumu,
Kukueleza harimu, yanohusu hizi enzi.

Dadangu taalamika, dunia chuo kigumu,
Na usipomakinika, ni shida kukihitimu,
Maadili kuyashika, kila siku uzuumu,
Maisha huwa magumu, usipotaadabika.

Dadangu nakuusia, uhifadhi wako mwili,
Ghulamu wakikujia, sitongozwe kwa sahali,
Usiwe kirukanjia, bali salia batuli,
Hadi wozwe mwanamwali, wakati ukiwadia.

Dadangu ukijiremba, kwa mapambo anuwai,
Kusahau kuupamba, moyo wako haifai,
Utalivutia bamba, la waume wakurai,
Upate stihizai, wakishakutinga mimba.

Dadangu kama hunaye, muhibaka maishani,
Mola akujaaliye, akuletee mwandani,
Na ijapo uko naye, penzi lenu lilindeni,
Mmtukuze Manani, mthibitike kwa yeye.

Dadangu hima kazana, uendapo darasani,
Jibaidi na fitina, na wanafunzi wahuni,
Fanya yanotakikana, uupite mtihani,
Ukifuzu masomoni, mambo yako yatafana.

Dadangu ujihadhari, mihadarati ni dhara,
Uraibu ni hatari, wa tambuu na sigara,
Mwili bangi huhasiri, kokeni nayo si bora,
Sifanye pombe sitara, kuitumia ghairi.

Dadangu mche Jalia, daima muweke mbele,
Mapenziye zingatia, uepuke mizingile,
Mema takuzidishia, ujazwe baraka tele,
Hutaziogopa ndwele, hazitakukaribia.

Dadangu u wa thamani, wewe bidhaa adimu,
Sijione kuwa duni, kwamba huna umuhimu,
Chapita cha marijani, kima chako muadhamu,
Moyoni mwako udumu, dhibiti wangu uneni.

No comments:

Post a Comment