Tuesday 30 July 2013

Jeshurun's Mind: Kiswahili na Mashairi


Duniani Twapita, Manzili Yetu Zayuni

 

Shairi hili ni fungu, la kuliwaza wafiwa,
Mnaohisi uchungu, liwagange kama dawa,
Kwa wafariji wenzangu, lina sifa maridhawa,
Duniani tunapita, manzili yetu Zayuni.

Rambirambi nazituma, kwa Milicenti Randa,
Kadhaka kwa yenu boma, na wote mnaopenda,
Nawaombea uzima, na roho ziso za inda,
Duniani tunapita, manzili yetu Zayuni.

Kakangu Napoleoni, na Adhiambo dadangu,
Nguvu nyingi jitieni, japo mnayo machungu,
Mola atawaauni, enyi wapendwa wenzangu,
Duniani tunapita, manzili yetu Zayuni.

Hakika ninayajua, yalokusibu Ajode,
Na vilevile Joshua, unayeipenda kode,
Angela nafanya dua, sifikwe na adeade,
Duniani tunapita, manzili yetu Zayuni.

Nasaha nawatolea, Akinyi na Dolphini,
Nanyi Samueli pia, Awiti na Liliani,
Ya hayati familia, tafadhali itunzeni,
Duniani tunapita, manzili yetu Zayuni.

Vijana waheshimiwa, kitunga nawavulia,
Kwani hamkuchelewa, mwenzenu kuhudumia,
Pindi mlipofikiwa, na habari ya tanzia,
Duniani tunapita, manzili yetu Zayuni.

Natoa zangu shukrani, kwako sayidi Obonyo,
Kwa nyingi zako hisani, na maneno ya maonyo,
Kwenda kwa Randa nyumbani, ulifwatwa unyounyo,
Duniani tunapita, manzili yetu Zayuni.

Pongezini vijulanga, Nyanchoka na Randiga,
Roho zetu mlikonga, kwa faraja zilonoga,
Akuku pia Wasonga, walizivalia njuga,
Duniani tunapita, manzili yetu Zayuni.

Mkono wa buriani, ameshatupa Aoko,
Maishaye duniani, yamekatiza mauko,
Tusisaili kwa nini, wakaa wa maziko,
Duniani tunapita, manzili yetu Zayuni.

Sunday 7 July 2013

Jeshurun's Mind: Kiswahili na Mashairi


Mawaidha Ya Maisha

Kila siku asubuhi, tumhimidi Jalia,
Daima tumstahi, kwa aliyotujalia,
Kiwemo staftahi, na kujua zake njia,
Ndiye atupaye nguvu, za kutafuta riziki.

Ni muhimu kukazana, katika yetu maisha,
Tena kukazana sana, pasina kulazimisha,
Tutendayo yatafana, na yatatuburudisha,
Tuusahau ugumu, uliokuwepo mwanzo,

Tusiwe walalamishi, kuguna hapa na pale,
Ikiwepo tashiwishi, katika hili na lile,
Tusiuzue ubishi, kwani hatutenda mbele,
Mabishano kizingiti, cha maendeleo mema.

Kila dakika muhimu, tusitumie visivyo,
Tusiandae karamu, kwa mambo yalo ovyo,
Ni busara kufahamu, tufanyapo tutakavyo,
Bila kuwa na mipaka, tutajuta baadaye.

Nakamilisha uneni, wa hili langu shairi,
Kwani nimeshabaini, kulirefusha si vizuri,
Basi shika usukani, nikwachie ushauri,
Utulivu maishani, hutoka kwake Mwenyezi.


(Mtunzi: Ruth Nderitu, Chuo Kikuu Cha Maseno; Mhariri: Dennis Mbae)

Jeshurun's Mind: Kiswahili na Mashairi


Umuhimu Wa Elimu

Elimu ina faida, hivyo jikaze kusoma,
Uwe kaka au dada, uwe baba au mama,
Jihimu kusoma kada, utetee chako chama,
Umuhimu wa elimu, huna kifani mwenzangu.

Uingiapo shambani, itukie hujasoma,
Huwezi kuwa makini, kwenye wako ukulima,
Jembe lako mkononi, litakuwa kiserema,
Umuhimu wa elimu, huna kifani mwenzangu.

Ukitazama angani, kisha uione ndege,
Ndaniye yu rubani, msomi asiye bwege,
Hupaa furufuruni, haendi segemnege,
Umuhimu wa elimu, huna kifani mwenzangu.

Wendapo mahakamani, utampata hakimu,
Ni stadi sheriani, kazi yake kuhukumu,
Alifuzu masomoni, hakuiiza elimu,
Umuhimu wa elimu, huna kifani mwenzangu.

Muda unapougua, wamwendea daktari,
Ambaye hukukagua, hupima ya mwili hari,
Mara yeye hung'amua, iwapo kuna hatari,
Umuhimu wa elimu, huna kifani mwenzangu.

Ufanyapo biashara, pasina bora elimu,
Utaipata hasara, kwa kutojua rakamu,
Walosoma tawahara, kwa kuelewa rajamu,
Umuhimu wa elimu, huna kifani mwenzangu.

Kituoni nimefika, kukujuza ufahamu,
Ya kuwa utadhikika, ukipuuza elimu,
Katu hupati fanaka, ukimbeza mwalimu,
Umuhimu wa elimu, huna kifani mwenzangu.

(Mtunzi: Elizabeth Achuman; Mhariri: Dennis Mbae)

Jeshurun's Mind: Kiswahili na Mashairi


Tuwathamini Wazazi 


Ewe kijana mwenzangu, nataka tusemezane,
Pamoja tupige gungu, yanotuhusu tunene,
Chiraze Mwenyezi Mungu, kadhalika tujuzane,
Kutothamini wavyele, huleta nyingi laana.

Miezi tisa tumboni, kakubeba wako nina,
Ukakaa mle ndani, kuishi ukakazana,
Kakuhuisha Manani, kwa kile kiungamwana,
Kutothamini wavyele, huleta nyingi laana.

Pindi ulipozaliwa, na kuja ulimwenguni,
Mama likupa maziwa, kakulaza kifuani,
Mno ulifurahiwa, wengi walikutamani,
Kutothamini wazazi, huleta nyingi laana.

Ulitokwa na udenda, karibu kila wakati,
Ukavalishwa ubinda, ili haja kudhibiti,
Wakakufundisha kwenda, na kusimama kititi,
Kutothamini wavyele, huleta nyingi laana.

Ulifanyiwa hisani, ukapelekwa skuli,
Wazazi wakajihini, welimike kulihali,
Wangengia izarani, ungeshia kuwa kuli,
Kutothamini wavyele, huleta nyingi laana.

Umeshakuwa mkubwa, sasa wabeza wazazi,
Ulopikiwa ubwabwa, umegeuka bazazi,
Licha ya ulivyobebwa, wawatusi waziwazi,
Kutothamini wavyele, huleta nyingi laana,

Mwenzangu nakuadibu, jiepushie balaa,
Mthamini wako abu, ujitenge na fajaa,
Unazo nyingi sababu, za kuwaonyesha taa,
Kutothamini wavyele, huleta nyingi laana. 

(Mtunzi: Eunice K. Kimbiri; Mhariri: Dennis Mbae)