Kiswahili na Mashairi


KANILEMAZA

Mwenzenu kanilemaza, na kunivaa moyoni,
Mengi yamenipendeza, siulize kwa nini,
Mengine ni miujiza, ameshushiwa mwandani.

Ukweli haufichiki, kajaaliwa imani,
Undani yeye hataki, penye kosa hubaini,
Umbile hamithiliki, bashasha za kila fani.

Mkweli kakamilia, anafahamu hisani,
Mpole zake tabia, si mtu wa ushindani,
Mzuri katimilia, aloazimu amini.

Anajua nampenda, moyoni ameamini,
Ameridhi kuniganda, katu hatubandukani,
Popote ninapokwenda, yumo mwangu mawazoni.

Mtunzi: Sihaba Juma




WAADVENTISTA WA SABATO WALIO FUFUTENDE (LUKEWARM SEVENTH-DAY ADVENTISTS)


1. Nandika waraka wangu, wende karibu na mbali,
Uwafikie wenzangu, mulio kila mahali,
Ameniagiza Mungu, niwadibu kulihali,
Enyi watunza Sabato, chungeni wenu mwenendo.

2. Sana mlibidiika, zile enzi za zamani,
Mkawa mnatajika, mbinguni na duniani,
Lakini mmegeuka, hamko tena makini,
Enyi watunza Sabato, chungeni wenu mwenendo.

3. Mumekuwa mwasusia, kukutana Jumatano,
Isomwapo Bibilia, na kwelezwa kwa mifano,
Nayo Ijumaa pia, hamwendi kwa mkutano,
Enyi watunza Sabato, chungeni wenu mwenendo.

4. Sabato inapofika, hamnazo mwajitia,
Hamwishi kushughulika, Mungu mwamkaidia,
Hivyo basi mwaruzika, kwa mbovu  zenu  tabia,
Enyi watunza Sabato, chungeni wenu mwenendo.

5. Mumezowea vibaya, kuchelewa Kanisani,
Hata hamuoni haya, mwenda mapema kazini,
Baadhi yenu wambeya, hutiana midomoni,
Enyi watunza Sabato, chungeni wenu mwenendo.

6. Licha ya kulimatia, kuwasili Kanisani,
Kelele huwapigia, walowahi Ibadani,
Mukichoka husinzia, na kwenda usingizini,
Enyi watunza Sabato, chungeni wenu mwenendo.

7. Ibadani mkitoka, mwafululiza nyumbani,
Mkiwa na uhakika, hamurudi Kanisani,
Huzidi kuhangaika, Siku ilo ya Manani,
Enyi watunza Sabato, chungeni wenu mwenendo.

8. Ijapo kutoa zaka, pamwe na dhabihu zenu,
Mikono yenu birika, mwampa Mola kununu,
Mkahiniwa baraka, na kukosa nyingi tunu,
Enyi watunza Sabato, chungeni wenu mwenendo.

9. Sinayo chuki na mtu, na mtu sina kinyongo,
Bali naisafi kutu, ya nyoyo na zenu bongo,
Kunoa silaha butu, za kiroho ndilo lengo,
Enyi watunza Sabato, chungeni wenu mwenendo.

10. Nahitimisha shauri, shairi nafupiliza,
Likiwa refu si zuri, kusoma na kusikiza,
Hapa basi nahiyari, beti kumi namaliza,
Enyi watunza Sabato, chungeni wenu mwenendo.

(Mtunzi: Millicent Randa, Jericho SDA Church, NAIROBI.   Mhariri: Dennis Mbae).



Happy Birthday!

1. Dada yangu biti Randa, najua nimekutupa,
Ukadhani nakutenda, ukawa watapatapa,
Nilikuwa nimekwenda, kutafuta cha kukupa,
Unapoiadhimisha, sikuyo ya kuzaliwa.

2. Nilipotafuta rinda, na kuzizengea kapa,
Wavaliazo makinda, kutoka bara Uropa,
Nilipata tu matunda, niliyotaka kukupa,
Ulipoiadhimisha, sikuyo ya kuzaliwa.

3. Ningekuwa na mabunda, ya noti haungekopa,
Tungelicheza kandanda, na kwenda jijini Jopa,
Jahazi ningeliunda, na kukuvulia papa,
Kila uadhimishapo, sikuyo ya kuzaliwa.

4. Ndege nyingi tungepanda, nauli ningeilipa,
Ningekutembeza Rwanda, kadhaka pale na hapa,
Tanzania tungekwenda, nikuonyeshe Mkapa,
Kila uadhimishapo, sikuyo ya kuzaliwa.

5. Umetimiza miaka, ishirini na mitatu,
Hiyo ni kubwa baraka, usiisahau katu!
Nakuombea fanaka, toka kwa Mungu na watu,
Unapoiadhimisha, sikuyo ya kuzaliwa.

 

Saratani Twakwapiza 


1. Ewe ugonjwa hatari, mbona hauna huruma?
Katu hautahayari, kitunyang’anya uzima, 
Saratani twakwapiza, jibaidi nasi sote. 

2. Hubagui wa kutesa, mayatima watuacha, 
Watuletea mikasa, hata wakembe mapacha, 
Saratani twakwapiza, jibaidi nasi sote. 

3. Wawahasiri watoto, na watu wazima pia, 
Makaliyo ni ya moto, daima twayahofia, 
Saratani twakwapiza, jibaidi nasi sote. 

4. Tiba yako mno ghali, hata kwao matajiri, 
Kuimudu ni muhali,  ukiwa mburumatari, 
Saratani twakwapiza, jibaidi nasi sote. 

5. Watuacha bila hela, watumiza kila siku, 
Wafaa kufungwa jela, utuondokee huku, 
Saratani twakwapiza, jibaidi nasi sote. 

6. Umefanya tuwe nyuma, hasa kimaendeleo, 
'Meua wenye hekima, tukakosa mema yao, 
Saratani twakwapiza, jibaidi nasi sote. 

7. Uraibu wa sigara, na vileo tuacheni, 
Tusile vilivyo dhara, viletavyo saratani, 
Saratani twakwapiza, jibaidi nasi sote.


(Mshairi: Eunice Kimbiri. Mhariri: Dennis Mbae)

 

Ufasaha Hudumani 


1. Mola usiyeshabihi, Mwenyezi twakuhimidi,
Twakutukuza Ilahi, madhali hivyo yabidi,
Kwa neema tumewahi, kuwa wako mashahidi,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.

2. Jumanne ndio siku, tulipofika Karura,
Zikatujaza shauku, za uongozini sera,
Sera ziso za udaku, zisizoleta hasara,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.

3. Siku iliyofuata, ndiyo hiyo Jumatano,
Vijana tulitakata, likaanza kongamano,
Sote tulifanya kwata, gwaride liso mfano,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.

4. Mambo mengi ya thamani, tumefundishwa vijana,
Uadilifu kazini, ni nguzo muhimu sana,
Hususa uongozini, ili kuwepo kufana,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.

5. Hayawani kama twiga, ngamia mchwa na tai,
Wanayavalia njuga, mambo yote ya uhai,
Tunapaswa kuwaiga, kuwabeza haifai,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.

6. Ewe mchungaji Juma, mgeni mheshimiwa,
Akurehemu Karima, upate kufanikiwa,
Ujazwe nayo hekima, uzidi kuinuliwa,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.

7. Ulifundisha wanyama, wanayo mafunzo tele,
Kwamba tukiwaandama, sote tutasonga mbele,
Kititi tutasimama, tuishi hata milele,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.

8. Mchungaji Okioma, Yehova akubariki,
Kwa kututendea mema, kutupa kile na hiki,
Mambo yote ulosema, kwayo tutajihakiki,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.

9. Kuwasahau siwezi, wachungaji wengineo,
Mlokuwa hapa juzi, siku zote hata leo,
Awafadhili Mwenyezi, na wote waaminio,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.

10. Nanyi vijana wenzangu, sikizeni kwa makini,
Matamu pia machungu, mtapata maishani,
Ngome yenu iwe Mungu, yeye mtumainini,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.

11. Kituoni nimefika, nawaaga kwaherini,
    Kutamka nimechoka, napisha yenu maoni,
    Yesu yuaja kumbuka, hilo tujue yakini,
    Ufasaha hudumani, Manani utujalie



Mahojiano kati ya Freddy Macha na Profesa Said Ahmed Mohammed, Mwandishi wa zaidi ya vitabu 30 vya Kiswahili.

 

Sehemu ya Pili


Kwa wasomaji wapya. Mwandishi Said A Mohammed keshaandika zaidi ya vitabu thelathini ikiwemo michezo ya kuigiza (tamthiliya), riwaya, mashairi na vitabu ya watoto. Riwaya yake maarufu, Asali Chungu, ilichapwa mara ya kwanza, 1976. Mwandishi aliyetopea, Adam Shafi, aliwahi kusema katika mahojiano na mhadhiri wa Kiswahili Ujerumani, Lutz Diegner, kwamba Asali Chungu ni miongoni mwa hazina kuu za Kiswahili na hupenda sana, kukisoma... Endelea...

Freddy Macha 
Riwaya zako tatu zimepishana miaka 36. Je kwanini, muda mrefu toka Utengano hadi Nyuso? Asali Chungu (1977), Utengano(1980) na Nyuso za Mwanamke (2010), Mhanga Nafsi Yangu (2012). Vile vile dhamira kuu inamwangalia mwanamke kwa macho na hisia za kumtetea. Mwandishi mwingine Mwafrika anayesimama upande wa kina mama (hasa vitabu vyake vya mwanzo) ni Msomali - Nuruddin Farah. Je, kwanini wanaume muwatetee wanawake? Kwani hawawezi kuandika wenyewe?  


Mwandishi Said A Mohammmed 
Kuandika riwaya au kazi yoyote ya fasihi kunahitaji wakati, utulivu na wiitisho wa ndani wa nafsi ya mwandishi. Huwezi tu kujilazimisha kufululiza. Kisha nadhani vita vya wanawake ni vita vya wanaume pia kama ilivyo kwamba vita vya wanaume ni vita vya wanawake. Kwa hali hii hakuna suala la kwa nini? Kwa bahati mbaya waandishi wanaume wachache tu ndio wenye msimamo wa ukombozi wa wanawake katika fasihi ya Kiswahili. Ama suala la wanawake kutoandika wenyewe wapo wachache katika fasihi ya Kiswahili wanaoandika hata kwamba hawajitetei. Jambo hili linashikamana na historia ya wanawake katika jamii zetu. Wanawake popote pale wamekuwa katika historia ya ukandamizwaji, je kwa nini tusiwatetee?.

Freddy Macha 
Sauti unayotumia kuelezea kisa chako katika Nyuso za Mwanamke ni tofauti na Utengano na Asali Chungu. Mtindo wa Nyuso ni wa “ki-maelezo” zaidi kuliko kutumia wahusika kama Semeni, Zuberi na Dude (Asali Chungu) na Maimuna, Maksudi na Shoka (Utengano). Je kwanini ukaamua kufanya hivyo?  


Wachapishaji wake mwanafasihi Said Mohammed wenye makao makuu Nairobi na ofisi mbalimbali Afrika Mashariki.  

Mwandishi Said A Mohammed
Kila kazi ya fasihi katika utanzu wake ni kama mtoto ambaye amezaliwa na mama na babake. Hawezi mtoto mmoja awe sawa na mtoto mwengine wa tumbo moja. Huu ni ukweli pia katika uandishi wa kubuni. Lakini sidhani kwamba simulizi yangu katika Nyuso za Mwanamke ni simulizi ya kueleza tu, yaani “telling or descriptive”, bali kwa sehemu kubwa ni ya kuonyesha “showing” kupitia wahausika wangu. Na kwa upande mwingine haiwezakani riwaya kuisimulia kwa mtindo mmoja bali kwa mshikamano wa mitindo miwili.

Freddy Macha 
“Nyuso..” imechukua muda mrefu sana kumshika msomaji kuliko vile visa vya mwanzo.Hadi ukurasa wa 44 ndipo kisa kinapoanza kujitokeza kwamba chamhusu mtu na mzazi wake. Mwandishi ana uhuru wa kuchagua mtindo wa kuelezea riwaya yake. Je kwanini ukachagua mtindo huu wa mafumbo mafumbo na kuchelewesha habari na maudhui? Je kadri mwandishi unavyoendelea kukomaa unashawishika kufanya majaribio ya ki fani? Na je, umepata “matokeo” au mrejesho nyuma gani kutoka kwa wasomaji wako kuhusiana na kisa hiki?

Mwandishi Said A Mohammed
Kama kweli wasomaji wote wanahisi kuchelewa kwa hadithi ya Nyuso za si hakika. Labda inaweza kuwa riwaya hii ina katika matapo (layers) mengi. Isitoshe, mhusika mkuu Nana ana tatizo la kuzungumza ndani ya nafsi yake na kuzungumza mwenyewe kwa mwenyewe, kwa hivyo mwanzo hakuna mgongano wa wahusika ambao unatazamiwa kumchangamsha msomaji. Nana ana tatizo linalomfanya aelezee yeye nani na kwa nini ametengana na mamake, jambo ambalo ni msingi mkubwa wa hadithi hii. Lakini hata magwiji wa riwaya wanazungumziwa kuwepo “purple colours” na uchangamfu katika kazi zao – yote mawili.  



Freddy Macha 
“Utengano” na “Nyuso” zina mlolongo wa maneno mapya au “magumu” ya Kiswahili. Huu ni mtindo mzuri sana wa kuendeleza lugha yetu.Si waandishi wengi wanaotupa “sherehe” kama hii. Labda tutegemee kwamba “Asali” ikichapishwa tena pia iwekewe “sherehe” , maana ina maneno mengi “magumu”?

Mwandishi Said A Mohammed 
Kwanza niseme kwamba Kiswahili kina utajiri mwingi lakini waandishi wachache wanasahau hivyo au hawataki kusikia wenzao wanavyosema na wanavyoandika. Pili, wazo lako nalikubali kwa ukamilifu.  


Freddy Macha 
Visa vyako huchimba undani wa wahusika kuonyesha maisha magumu lakini hapo hapo kutekenya ndoto njema na fikra za wanadamu. Ukurasa 118 (Asali) tunaonyeshwa Dude alipopata ahueni baada ya kufarijiwa na mke wa Zuberi. Mwandishi unasema: “Ata! Dude hataki tena kufa; anataka aishi.Ni nani asiyetaka kuishi?” Utengano hali kadhalika.Bi Kocho anaonyesha ari ya kike akiongea na Farashuu (uk 61): “Sifi kwa ufukara, nikafa kwa kuteswa na mtu. Wakati wa kuogopa umekwisha. Hata kama Maksuudi angalikuwa Mzungu.” Na “Nyuso” hali kadhalika (uk 39): “Nilihisi kwamba haki ya kuwa huru ni haki yangu ya kwanza ya msingi.” Je, lengo na msimamo wako mwandishi kuonyesha jazba ya wanadamu na kwamba ushindi ni kheri yetu kuliko fikra za kushindwa na kukata tamaa na maisha? Au imetokea tu?

Mwandishi Said A Mohammed 
Unajua kutaka tusitake, kila mwandishi ana msimamo na falsafa yake. Mimi siwezi kuwafanya wahusika wangu wakate tamaa. Bila ya tamaa binadamu hawezi kujikomboa. Ukweli ni kwamba bado tunatawaliwa na tena vibaya vibaya.  



Freddy Macha 
Riwaya hizi tatu zimeelezewa ndani ya maisha ya Visiwani peke yake. Lakini mwandishi umetembea na kuishi mazingira mengine mfano Kenya, Tanzania Bara na Ulaya. Kwanini huangalii huko pia kama ulivyofanya katika hadithi yako fupi “Tazamana Na Mauti” (Damu Nyeusi) inayoangalia maisha ya London?

Mwandishi Said A Mohammed
Hadithi mara nyingi huja na kuendana na mandhari (setting) yake. Baada ya kukaa nje ya Zanzibar na Tanzania nimepata uzoefu wa nje, kwa hivyo soma kazi kama Baba Alipofufuka, Dunia Yao, Mhanga Nafsi Yangu n.k, utaona kwamba nimefaidikia kimaudhui na kimandhari yanayokamatana katika uwili mmoja. Si kazi zangu zote ni za nyumabani tu.

Freddy Macha
Kifani una lugha ya kipekee inayochora mandhari, wahusika, hisia, mazingira. Mifano iko mingi sana – ila tuchague michache ndani ya “Utengano” na “Asali” zinavyochambua mazingira ya maskini- kilabuni (Utengano, uk 138-143 ) ambapo wanawake wawili – Maimuna na Kijakazi wanavyogombana. Hapa umeshika taji la kukionyesha Kiswahili kilivyo kitamu: “Kijakazi mwenye tabia ya uso wa samaki usiosikia viungo”; “Shoka alitia pamba masikioni”; “Nani anayeshtua watu akitupiwa mbwa hamtaki”; “Kijakazi alijitazama akajiona kapwaya kweli”; “Alikua shetani na aliweza kummeza yeyote.” Na kadhalika. “Asali Chungu,” inayachora maisha ya wananchi kwa undani. Kama wakati Semeni akijipamba. Uk 42 : “Baadaye alikunja miguu yake akaanza kuisinga kwa baki ya mafuta yaliyoroa mikononi mwake. Akarejesha zana zake chumbani na kurudi kukaa kwenye kiti cha marimba pale pale kwenye baraza. Alikua kakaa kwenye kile kiti, kinyume mbele, kajivuta nyuma na kukimwaya kiuno chake upande wa ukutani. Kifua na mikono ikalalia kiegemeo cha kiti, kichwa chake kimeelemea kwenye mikono yake aliyoipachika pamoja; akawa anamwangalia Pili aliyejitia hajamwona, anamfundika kijakazi mkia wa mwisho.” Je, una nini la kuwafundisha waandishi wachanga wanaokua sasa hivi namna ya kuyasifia na kuyapamba na kuyachora vizuri mazingira wanayoyaandika. Waandishi wengi vijana leo wanaandika michezo ya sinema, wanaandika tenzi za rapu (Bongo Flava) wanaandika hadithi fupi fupi. Ila mara nyingi hawajaonyesha mazingira kitaswira. Nini siri wanayoikosa? Ukiacha kipaji yaani.

Mwandishi Said A Mohammed
Kwanza wakipende Kiswahili, pili, wakisikilize na tatu wakisome kutokana na wale wanaokipenda Kiswahili. Wakubali kuiga, maana wigo si mbaya iwapo utatumika kwa kufunguka tu.

Freddy Macha 
Tuangalia mambo mawili pia yanayohusu lugha. Kwanza tueleze vipi ukaunda misemo mizito kwa maneno machache. Yanatoka wapi? Mfano: Nyuso (Sura 7; uk 70); “Maiti kasoro nukta.” Asali (Sura 11; uk 143) : “Ulimwengu ni mchafu. Je, yeye mlimwengu awe vipi?” Asali (Sura 8; uk 101) “Mungu haombwi; hutoa.” Utengano (Sura 10; uk 118 ) : “Bora nusu ya shari kuliko shari kamili.” Pili, tusaidie tafsiri ya maneno na misemo ya visiwani ambayo haieleweki kwa baadhi ya wasomaji wa bara: “Sherehe za wana kindakindaki” (Asali, Sura 12; uk 159) “Kuruka adi-mfundo” (Asali, Sura 8; uk 111) Je ni “andasa” au “andis”? (Asali, Sura 4; uk 50) “Hapendi, hataki, hajali wala habali” – (Utengano, Sura 1; uk3) “Mkareti” (Utengano, Sura 2; uk 20)

Mwandishi Said A Mohammed 
Nafikiri misemo na maneno hayo hapo juu yanatokana na upeo wangu wa kubuni na ukwasi wa lugha nilioupata katika utamaduni wangu. Ndio ule utamu wa lugha ulioutaja hapo juu. Mwandishi lazima awe mweledi na mwepese wa kutumia maneno na misemo yenye kuvutia na kushangaza. Mbali na hayo mwandishi lazima asikilize watu wanavyosema katika jamii husika na utamaduni wake unaotoa nafasi ya kuunda misemo na kauli za mvutio. Kindakindaki ni mtoto wa mtu mkubwa kama vile mfalme. Adimfundo ni aina ya mchezo wa kuruka vyumba vilivyochorwa ardhini. Neno andasa ni nomino na andis(i) ni kitenzi. Hapendi, hataki, hajali wala habali ni kauli ya msisitizo wa kutopenda. Mkareti ni aina ya mmea wenye mbegu ngumu kama mawe na pia unazungukwa na miba.  


Profesa Said A Mohammed, alistahafu kazi ya kufundisha Kiswahili vyuo vikuu mbalimbali duniani, mwaka jana.


Samahani Wanangu

 

Na Mrisho Mpoto akimshirikisha Maunda

 


Taabu, maisha kila siku,
Maajabu mchana hata usiku,
Haya ndio maisha yetu, 

Samahani sana wanangu, wanangu wapendwa salamu,
Leo hizi ni salamu zangu za dhati, salamu za upendo,
Salamu zitokazo ndani, mvunguni mwa moyo wangu,
Salamu zilizobeba dhati ya nafsi yangu,
Salamu adimu, ulimwenguni tunaoishi.

Nisameheni wanangu, moyo wangu umenituma barua,
Niwaandikie, wana na vijana  wangu,
Ikikufikia, mweleze na mwenzako,
Tuanze upya, tusahau jana yetu,
Tufunge ukurasa wenye inda, ubinafsi na dhuluma,
Tugeuke tuyape mgongo, yabaki historia,
Amini, samahani yangu ni nuru wa maisha yenu.

Wanangu, niandikapo barua hii,
Najua mko mahala fulani,
Ama ni asubuhi, jasho likiwatiririka,
Kwa kuangalia “pornography” kwenye internet café,
Baada ya kutoroka shuleni,
Si ajabu pia kuwa ni usiku wa manane,
Mmegeuka bidhaa zinazotembea nusu uchi, mkifukuzana na polisi,
Rambo mkononi, nao hawajapata kujua mmefikaje pale,

Na pengine, licha ya umri wa miaka kumi na mbili mko leba,
Mkisubiri ule wakati wa uchungu, sauti ya muuguzi ikikwambia,
Sina nauli, daktari kando ya kitanda akinung’unika,
Ada ya shule ya mwanaye kipenzi.

Wanangu, pengine ni usiku kati,
Mko kwenye “party”  ya kucheza uchi,
Ujira ni pakiti ya sigara,
Au labda mko shuleni chini ya miti mkisoma,
Mliopo kwenye vyumba mmeshonana mithili ya siafu,

Yawezekana kuwa ninapoandika waraka huu,
Mko majalalani mkichakuachakua vifusi vya taka,
Kama kuku wa kienyeji,  kutafuta makopo ya kuchezea,
Ama mwacheza mpira wa makaratasi vichochoroni,
Maana uwanja wenu umezungushwa mabati,
Na kuandikwa: “Mbwa mkali”, kisha ujenzi wa Casino.

Wanangu, lakini pengine mmejikongoja mpaka sekondari,
Maisha ya manamba ndio staili yenu, bila mikiki hakuna lishe,
Wakati nyinyi, nyoyo zenu zimebeba visasi na risasi,
Wenzenu wamebeba vifaa na zana, kuelekea sayari ya Mars,
Mmeshindiliwa hasira, mmebugizwa chuki,
Mkaombewa ibada ya ukatili, na roho wa ukatili akawabariki,
Sekunde hii damu ikitiririka, kwa shangwe na mori mnarukaruka,
Poleni sana wanangu, 

Taabu, maisha kila siku,
Maajabu mchana hata usiku,
Haya ndio maisha yetu, 

Miongoni mwenu njaa imeshikana na ngozi yenu,
Mbavu zenu zajianika mithili ya chanuo la mti,
Wakati huu nyinyi mkisoma waraka huu,
Wengine wanafanya mazoezi ya kunyanyua vyuma,
Kabla ya kupora cheni na  mikoba ya simu,
Wapo pia walioketi vijiweni wakiandika mabango:
“Heri kuwa mbwa Ulaya kuliko kuwa mwana wa nchi,”
Maana ardhi yenu imekuwa Jehanamu.

Wanangu, kweli hatamu ikishikwa punda sharti aende,
Sauti yenu imenifikia, nimeisikia nitawafikia,
Popote pale muwapo sekunde hii,
Wekeni taswira yenu mpya ya baba yenu mbele yenu,
Itazameni ikitiririka machozi ya majuto na upendo,
Machozi haya yameanza safari ndefu,
Yakilainisha pua zilizoona kinyaa kila mlipopaaza sauti,
Yakilainisha midomo iliyowabeza na kuwanunia na kuwafokea,
Yakitiririka zaidi hadi kifuani,
Kulainisha mioyo migumu iliyosisitiza nyinyi ni Taifa la kesho,
Pasi kujua kesho hujengwa na leo,

Tena zaidi machozi yalainisha mikono iliyowasukumia mbali,
Nayo ikawakumbatia na kufungua ukurasa mpya,
Sitasubiri, sitasubiri mpaka uchaguzi,
Ili mnibebe kwa pato la sahani ya pilau,
Kisha nikawatosa kama maganda ya miwa,
Japo niko mbali, anzeni kuhisi joto langu,
Isikieni sauti yangu ikiwanong’oneza,
Narudi kwenu enyi vijana mliolemewa na mizigo,
Furaha yangu kamili yategemea furaha yenu,
Samahanini wanangu, nawatakia maisha mema. 

Taabu, maisha kila siku,
Maajabu mchana hata usiku,
Haya ndio maisha yetu,


Mahojiano kati ya Freddy Macha na Profesa Said Ahmed Mohammed, Mwandishi wa zaidi ya vitabu 30 vya Kiswahili.

Sehemu ya Kwanza





Freddy Macha: Profesa Said, umeandika vitabu vingi. Ama kweli wewe ni hazina ya fasihi ya Kiswahili ambaye hujapata heshima inayokustahili. Najua hupendi kusifiwa – lakini lazima tukuthamini ungali hai maana wewe fahari yetu Waswahili. Hata ukiweka neno “Tanzanian Novelists”, “Zanzibar Writers”, au “Tanzanian Writers” katika Wikipedia hutajwi. Unadhani kwanini wengi hasa Tanzania bara na visiwani hawakufahamu ipasavyo?


Mwandishi Said A Mohammed:
Kama nilivyokueleza katika mkumbo wa masuali uliyoniuliza mwanzo hapo kitambo, Watanzania na zaidi Wazanzibari hawana utamaduni wa kusoma vitabu vya fasihi. Kwa hivyo hawajapata ari wala mwamko wa kujali na kuthamini fasihi yenyewe na waandishi wake. Kweli kuna wachache ambao wanatangazwa katika vyombo vya mawasiliano, lakini mimi simo katika orodha ya waandishi hao. Hili ni suala la vyombo vya habari ambavyo mara nyingi huwatukuza wale ambao wanataka wao watukuzwe. Vilevile kuna wasanii wanaopenda kujipeleka mbele ili wasikike na hata kuwa na fikra kwamba waandishi wengine wadidimie. Kwa bahati mbaya au labda kwa bahati nzuri, mimi si mtu wa kimbele mbele. Naamini sana maneno ya wahenga kwamba Kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza.



Katika dunia ya sasa kujipeleka mbele ili usikike bila umakinifu, ndilo jambo linaloharibu mambo mengi ikiwemo sanaa ya lugha. Vipawa vinadharauliwa na sanaa tunazokutana nazo ni sanaa zinazokuzwa tu bila ya kupitiwa kwa kina na kujadiliwa. Chambilecho, gwiji wetu wa fasihi, Profesa Ebrahim Hussein, hakuna fasihi tena kwa maana ya fasihi. Hakuna wasomaji wazingatifu. Hakuna uhakiki kwa maana ya uhakiki. Kuna fikra ya kwamba chochote kile ni sawa. Shairi, riwaya, hadithi fupi au tamthilia ikiwa ina sura ya tanzu inayohusika, basi ni fasihi tu kwa maoni ya wengi. Fasihi haipo. Wasomaji hawapo. Umakinifu wa fasihi haupo. Uhakiki umepotea. Hata wale ambao tunawatarajia kufanya hivyo hawashughuliki na kusoma, kuandika, kuhakiki na kuzitangaza kazi za fasihi ya Kiswahili. Sisi waandishi hatuwezi kujitetea. Wanaojitetea na kuwaponda wenzao ndio katika hao wanaowekwa mstari wa mbele na wanaojitapa kuwa wanajua hata kuandika kazi za waandishi wenzi wao.




Freddy Macha:
Kuna dhana inayodai ili mwandishi ajulikane labda aanzie uandishi wa habari, ajenge jina kihivyo kama walivyofanya baadhi ya waandishi maarufu duniani mfano: Gabriel Marquez (Colombia) , Ernest Hemingway (Marekani) au afungwe jela kama Wole Soyinka (wakati wa vita vya Biafra 1967-1970) na Ngugi Wa Thiong’o (Kenya, 1978). Hapa tunatumia neno “kujulikana” si kwa maana mbaya ya kutaka umashuhuri bali kutathmini wepesi wa wasomaji kuzijua, kuzithamini na kuzipenda kazi za mtunzi. Mathalan, Watanzania wengi wa kizazi kilichozaliwa baada ya mwaka 1970 wanamfaham marehem Elvis Musiba sana kutokana na tungo zake za mtindo wa kiupelelezi kuliko marehem Said Muhammed Said Abdulla aliyemtangulia kwa mtindo huo huo.


Mwandishi Said A Mohammed:
Suala halina ukweli kamili. Kuna mamilioni ya waandishi ambao hawajui hata maana ya uandishi habari na wengi katika hao ni waandishi wazuri wanaosifika na wako wazuri ambao hawajasifika kwa sababu hawajapewa nafasi ya kutangazwa katika vyombo vya habari. Nao hawapendi kujitokeza kifua mbele kwa kulazimisha kazi zao kuwa nzuri.



Freddy Macha:
Tukiendelea na mada hii hii. Waandishi wa vizazi mbalimbali wamefahamika kwa njia tofauti. Linganisha waandishi wa kizazi cha ukoloni na miaka michache baada ya ukoloni, mfano Mathias Mnyampala, Shaaban Robert, Muhammed Said Abdullah, Saadan Kandoro, Faraji Katalambula, nk- waliothaminiwa kwa kazi zao. Vitabu vyao viliuzwa madukani na hapo hapo kutumika mashuleni. Linganisha awamu hiyo na ile ya miaka ya 1970 kuendelea: Mohammed S. Mohammed, Adam Shafi, Euphrase Kezilahabi, Ebrahim Hussein nk, waliojiingiza ama katika mashindano kwanza (Mohammed Suleiman na “Kiu” -1970), Adam Shafi (tuzo la Uandishi Bora1998) au kupitia sanaa za maonyesho (Ebrahim Hussein). Kuanzia hapo mambo yalibadilika kabisa – waandishi wa vizazi vya miaka 1980 kuendelea walijenga majina kwa kujitangaza wenyewe kwa kutumia vyombo vya habari, makampuni waliyounda. Akina Kajubi Mukajanga, Hammie Rajab, marehem Ben Mtobwa, na mwandishi anayesomwa sana na vijana sasa hivi – E Shigongo – ambaye amewahi kuchapisha vitabu India-na shirika lake la habari na blog- Global Publishers. Hawa waliamua kuingia mitaani.


Mwandishi Said A Mohammed:
Kweli wakati au enzi ya wakati fulani na mambo yake yanaathiri sio tu fasihi, bali thamani ya fasihi, maudhui yake, fani yake, waandishi wake na kadhalika. Kwa maoni yangu wakati huu tulionao ni wakati wa upujufu mkubwa hasa katika dunia ya tatu. Wasomi hawana tena msimamo seuze watu wa kawaida. Pesa inatawala, tena inatakikana ipatikane bila ya kutoa jasho. Kila kitu kinauzwa na watu hawajui kuchagua au kutathmini vitu vyenye hadhi au pengine wanajua lakini hawana pesa za kununua vitu vyenye hadhi. Kwa hivyo tunaambukizana upotofu wa mambo na hatimaye hatutambui tunafanya nini. Kujijengea kampuni na kuuza vitabu vyake mtu ni jambo linawezekana na kwa kweli tunaliona, lakini mimi nadhani hakuna vipimo vizuri vya mtu anayefanya hivyo. Yeye mwenyewe aandike, tena avipitie mwenyewe, avihariri mwenyewe, atambue uzuri na ubaya wa kazi zake yeye mwenyewe na baadaye afyatue vitabu kama matofali, basi wanaonunua vitabu vyake lazima wawe na mushikeli. Kujitangaza na hata kutangazwa kwa maana ya kukuzwa tu na watu fulani hakuna maana ya kwamba hakuna wengineo wanaoandika, tena wanaoandika ambao wana vipawa vikubwa zaidi. Kuepuka utunzi wa kuuza badala ya kujiuza ndiko kunakopelekea fasihi ya Kiswahili idharauliwe na ipuuzwe duniani.



Freddy Macha:
Je tunaweza kusema wewe kama mwandishi uliyeamkia miaka ya mwisho ya Sabini, ulitegemea tu vitabu vyako kuingia madukani na kusomwa bila kuingia madukani kama Shigongo na Ben Mtobwa – Mungu amrehemu – waliouza vitabu kama miwa, miswaki, nyama choma na nyanya?


Mwandishi Said A Mohammed:
Ndiyo, mimi niliandika na mpaka sasa naandika kwa kutegemea vitabu vyangu kuuzwa madukani, sababu ni kwamba sitaki vitabu vyangu niviuze kama miwa, miswaki, nyama choma na nyanya. Lengo langu sio pesa, bali ukweli na umahiri wa kuandika ingawa hata na mimi nathamini na nazitaka pesa kama wenzangu.



Freddy Macha:
Halafu kuna suala tulilozungumzia mwaka jana la kupitisha vitabu mashuleni kwanza ndipo visomwe au kuuzwa. Hapa tunaangalia pia tatizo linalowakumba wachapishaji na soko zima la vitabu vya Kiswahili. Wewe mwenyewe umeandika vitabu vingi katika medani hii…


Mwandishi Said A Mohammed:
Ingawa mimi nimeandika vitabu vingi mpaka sasa, vichache tu ndivyo vilivyopata nafasi kuingia mashuleni. Na hivyo vilivyoteuliwa kuingia shule vilisomwa mwanzo kabla ya kusomwa kwa madhumuni ya elimu shuleni.


Freddy Macha:
Upo usemi ulioenea kwamba waandishi wa Kiswahili toka enzi za ustaadh Shaaban Robert mwenyewe hadi leo hawawezi kuuza kazi zao duniani kama wasipoandika lugha za Kizungu. Hapa tutoe mifano ya William Mkufya (Wicked Walk), Ismail Mbise (Blood On Our Land), M G Vassanji na Abdul Razak Gurnah. Profesa Gurnah na Vassanji (ambao wamehama Afrika Mashariki miaka mingi sana) wameshashinda tuzo kibao za kimataifa kutokana na kuandika Kiingereza. Je ndiyo suluhisho? Mbona Watanzania na wasomaji wa Kiswahili hawawafahamu hawa wawili (Vassanji na Gurnah) hasa nao wamechangia sana kujenga fasihi ya Kiafrika muda mrefu?



Prof Abdul Razak Gurnah, mwaandishi wa Kitanzania anayeishi nje na aliyeshajenga jina kimataifa.

Mwandishi Said A Mohammed:

Mimi ni mmojawapo ambaye ninaamini kuandika kwa lugha apendayo na kwa mtindo auchaguao ni haki ya mwandishi. Sababu za kuchagua lugha inakamatana na mtu kuandikia watu gani au kwa sababu gani. Wengine wanaandika kwa fahari ya lugha yao, utamaduni wao na uelevu wa watu wao ambao wangeweza kuisoma kazi husika na kuitafakari. Wengine wanaandika kwa lugha ya kigeni kwa sababu wanadhani kuwa lugha ya kigeni ina mvuto mkubwa kwa kazi ya fasihi, tena lugha ka ya Kiingereza husifiwa na kutoa hadhi kubwa kwa waandishi.





Mimi nimo katika kundi la mwanzo, yaani kuandika kwa maana ya kukitukuza Kiswahili, fasihi na utamaduni wake. Pia kuwapa fursa wananchi walio wengi na ambao hawakijui Kiingereza lakini wana nafasi ya kufurahi sanaa yao lugha yao na kubwia fikra za raia wenzao ambao ni waandishi. Zaidi ya hayo, si kweli kwamba wanaoandika kwa Kiingereza wanathaminiwa au wanapata pesa nyingi. Inatia moyo kwamba duniani fasihi haiandikwi kwa Kingereza tu, bali Kichina, Kirusi, Kijerumani, Kifaransa, Kiholanzi n.k

 

Maneno Yanayotumika Sana Maishani Mwetu


Kwa hisani ya Jukwaa la Kiswahili na Waswahili Halisi


1. Password - Nywila
2. Scanner - Mdaki
3. Mouse - Kisakura au Kipanya
4. Flash disk - Diski mweko
5. Computer virus - Mtaliga
6. Device - Kitumi

7. Processor - Kichakato
8. Monitor - Muwazi
9. Sensor - Kisimbuzi
10. Nutrients - Virutubisho
11. Memory card - Kadisakima
12. Resistor - Kikinzani
13. Photocopier - Kinukuzi
14. Duplicating machine - Kidurufu
15. Microwave - Tanuri ya miyale
16. Floppy disk - Diski tepetevu
17. Key board - Kicharazio
18. Slot - Upenyu
19. Juice - Sharubati
20. Force of gravity - Kani ya mvuto
21. Certificate - Astashahada
22. Diploma - Stashahada
23. Degree - Shahada
24. Masters - Uzamili
25. Phd - Uzamifu.


 

Siku Ya Vijana Wakubwa Na Wa Marika


Mungu mwenye mamlaka, twakuhimidi Rabana,
Hufanya unavyotaka, hauna wa kufanana,
Roho zetu e Rabuka, kwako twaweka  amana,
Leo siku ya vijana, wakubwa na wa marika.

Pongezini Manasara, mlokongamana hapa,
Hususa nyie vinara, kwa nafasi mlonipa,
Nawaombea busara, mjazwe bila kukopa,
Leo siku ya vijana, wakubwa na wa marika.

Pulikeni niweleze, yaliyomo mtimani,
Rai yangu tujikaze, Injili tuhubirini,
Nguvu zetu tusisaze, hadi tufike mbinguni,
Leo siku ya vijana, wakubwa na wa marika.

Nasema nawe Owiti, uitwaye Imanweli,
Jua si mwingi wakati, wa kueneza Ukweli,
Hivyo simama kititi, uiwaidhi Injili,
Leo siku ya vijana, wakubwa na wa marika.

U wapi ndugu Hagai, nikupe yangu nasaha?
Uliopewa uhai, siufanyie mzaha,
Kifanywa sitihizai, dumisha yako sitaha,
Leo siku ya vijana, wakubwa na wa marika.

Nanena na dada zangu, ninyi Achola na Linda,
Yakiwapata machungu, himilini mtashinda,
Mkimtukuza Mungu, kwenu Yeye ataganda,
Leo siku ya vijana, wakubwa na wa marika.

Waloko ughaibuni, wapewe zangu salamu,
Wambiwe humu nchini, kuwaona tuna hamu,
Twaomba kwake Manani, walindwe na hali ngumu,
Leo siku ya vijana, wakubwa na wa marika.

Ndugu Saya twashukuru, kwa vifijo na kwa kwata,
Umetwangazia Nuru, Neno njema umeleta,
Shetani hatakudhuru, nyotayo itatakata,
Leo siku ya vijana, wakubwa na wa marika.

Iwapo sikukutaja, si kwamba huna maana,
Siwezi nikakuchuja, mimi nakupenda sana,
Wako wengi walokuja, silijui lako jina,
Leo siku ya vijana, wakubwa na wa marika.

Tuyaanzapo Makambi, Rabi tupe nguvu zako,
Yasikilize maombi, ya wanao wa Yeriko,
Uwepushie mawimbi, na yote misukosuko,
Leo siku ya vijana, wakubwa na wa marika.

Kituoni nimefika, nawaaga kwaherini,
Kutamka nimechoka, napisha yenu maoni,
Yesu yuaja kumbuka, hilo tujue yakini,
Leo siku ya vijana, wakubwa na wa marika.

(Mtunzi: Felix Akuku, Jericho SDA Church, NAIROBI. Mhariri: Dennis Mbae).


Mausia Kwa Kila Kijana Mwanamke 


Dadangu ninayeenzi, pokea zangu salamu,
Popote ulipo mwenzi, nakujali ufahamu,
Hivyo nikiwa mtunzi, ninayo kubwa hamumu,
Kukueleza harimu, yanohusu hizi enzi.

Dadangu taalamika, dunia chuo kigumu,
Na usipomakinika, ni shida kukihitimu,
Maadili kuyashika, kila siku uzuumu,
Maisha huwa magumu, usipotaadabika.

Dadangu nakuusia, uhifadhi wako mwili,
Ghulamu wakikujia, sitongozwe kwa sahali,
Usiwe kirukanjia, bali salia batuli,
Hadi wozwe mwanamwali, wakati ukiwadia.

Dadangu ukijiremba, kwa mapambo anuwai,
Kusahau kuupamba, moyo wako haifai,
Utalivutia bamba, la waume wakurai,
Upate stihizai, wakishakutinga mimba.

Dadangu kama hunaye, muhibaka maishani,
Mola akujaaliye, akuletee mwandani,
Na ijapo uko naye, penzi lenu lilindeni,
Mumtukuze Manani, mthibitike kwa yeye.

Dadangu hima kazana, uendapo darasani,
Jibaidi na fitina, na wanafunzi wahuni,
Fanya yanotakikana, uupite mtihani,
Ukifuzu masomoni, mambo yako yatafana.

Dadangu ujihadhari, mihadarati ni dhara,
Uraibu ni hatari, wa tambuu na sigara,
Mwili bangi huhasiri, kokeni nayo si bora,
Sifanye pombe sitara, kuitumia ghairi.

Dadangu mche Jalia, daima muweke mbele,
Mapenziye zingatia, uepuke mizingile,
Mema takuzidishia, ujazwe baraka tele,
Hutaziogopa ndwele, hazitakukaribia.

Dadangu u wa thamani, wewe bidhaa adimu,
Sijione kuwa duni, kwamba huna umuhimu,
Chapita cha marijani, kima chako muadhamu,
Moyoni mwako udumu, dhibiti wangu uneni.

I-M-A-N-I


Imani ni uhakika, wa yanayotarajiwa,
Ni kuzidai baraka, kana kwamba zimekuwa,
Ni kuyapinga mashaka, muda unajaribiwa,
Imani ni kutulia, na kumwamini Jalali.

Maombi bila imani, ni muhali kujibiwa,
Shaka likiwa moyoni, sala zetu huzuiwa,
Kumfikia Manani, tukakosa majaliwa,
Imani ni kuamini, hitaji limetimizwa.

Abramu baba imani, twastahiki kumwiga,
Alihajiri Hanani, jamaaze kawaaga,
Akakaa ugenini, pasi na kuwa na woga,
Imani ni kumtii, na kumpa Mola vyote.

Nuhu naye kadhalika, ni shujaa wa imani,
Ilani yake Rabuka, aliiweka moyoni,
Hivyo akanusurika, na watuwe duniani,
Imani ni kusadiki, maneno yote ya Mungu.

Imani bila matendo, imeshakufa yakini,
Matendo yakiwa kando, ni hasara kuamini,
Lisipodhihiri pendo, imani yafaa nini?
Imani ni kuyatenda, mapenzi yake Mwenyezi.


Mapenzi Ni Kikohozi, Hayawezi Kufichika

 

Mapenzi ulimwenguni, yaliletwa na Muumba,
Bustanini Edeni, Manani akayapamba,
Na tangu hizo zamani, yakawa ni kumbakumba,
Huwatoa kitweani, wajaliwao wachumba,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika.

Mapenzi kitu azizi, kwa nisai na rijali,
Katu hayana mjuzi, ulamaa wala nguli,
Huathiri mabazazi, wakawa wenye adili,
Kama lilivyo duwazi, zi wazi zake dalili,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika.

Mapenzi kama majani, popote pale huota,
Hayazibagui dini, lugha na za watu kata,
Hata rangi ya ngozini, si kitu yanaponata,
Huwatia upendoni, matajiri na wakata,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika.

Mapenzi huwa utumwa, pindi yakilazimishwa,
Waathiriwa huumwa, bilashi hushughulishwa,
Huku huba wakinyimwa, na wazi kuaibishwa,
Kwa uchungu hufumwa, mwisho nje hurushwa,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika.

Mapenzi pia huvunda, na kujawa na vituko,
Udhanipo wewe chanda, na yeye ni pete yako,
Ukawa unampenda, kumuona yu mwenzako,
Kumbe unafuga donda, moyowe hauko kwako,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika.

Mapenzi yalo kiboko, kuyapata ni vigumu,
Usifikiri hayako, mahaba yalo matamu,
Huleta msisimko, ladha ya asikirimu,
Hayazui chokochoko, hung'aa kama nudhumu,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika.

Mapenzi utathamini, ukiwa unayajua,
Utamuenzi mwandani, hata akikuzuzua,
Utapenda zake mboni, na macho ya kurembua
Na umbo la wastani, nyonda likikuzingua,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika.

Mpenzi uloridhia, kumuacha si rahisi,
Maradhi ukiugua, yeye kwako huwa nesi,
Na dozi hukupatia, hudumani ni mwepesi,
Kwa unalohitajia, hutamki anahisi,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika.

Mapenzi ili yadumu, kuyatunza ni faradhi,
Uzinzi huwa ni sumu, huleta mengi maradhi,
Waminifu ni muhimu, hubaidi na kuudhi,
Ni hayo natakalamu, kitunza hutabughudhi,
Mapenzi ni kikohozi, hayawezi kufichika.

 

Wakenya, Kutozuru Kenya Kwa Obama Kwawashiani?


Wakenya mbona mwawashwa, na ziara ya Obama?
Bure mnababaishwa, naye kutowatazama,
Na Mungu huwa twalishwa, twavishwa twawa salama,
Mtumai cha nduguye, hufa hali masikini.

Siku nenda siku rudi, mwatazama Magharibi,
Mnasema yawabidi, kwani kuna mahababi,
Kuwadibu sina budi, mkimkinai Rabi,
Mtumai cha nduguye, hufa hali masikini.

Japo Kenya asiliye, Obama haithamini,
Alikotoka abuye, kwake kitongoji duni,
Msimtumai yeye, msijishushe thamani,
Mtumai cha nduguye, hufa hali masikini.

Wakati aliposhinda, uchaguzi Marekani,
Waziwazi alidinda, kuwazuru kumbukeni,
Na ingawa mlikonda, kwake mlitumaini,
Mtumai cha nduguye, hufa hali masikini.

Muhula wa kwanza wake, alitembea Afrika,
Mkakaza macho kwake, mno mkafurahika,
Lakini akenda zake, mkawa mwasikitika,
Mtumai cha nduguye, hufa hali masikini.

Obama sasa yuaja, tena barani Afrika,
Mmezidisha harija, kwani Kenya hatafika,
Maizini zenu haja, wa kutimiza Rabuka,
Mtumai cha nduguye, hufa hali masikini.

Komeni kutegemea, mwanadamu asodumu,
Kwani yeye hupokea, machunguye na matamu,
Aghalabu hulegea, hayo ninyi mfahamu,
Mtumai cha nduguye, hufa hali masikini.

Beti nane zimetimu, nahitimisha shairi,
Kwenu liwe talasimu, nilosema likariri,
Tena liwatie hamu, mmrudie Qahari,
Msitumai vya ndugu, msijefa masikini.

 

Baragumu Inalia, Ulimwengu Pulikiza


Bismila nakadimu, jinale Muumba wangu,
Tangu abadi hudumu, mfanya nchi na mbingu,
Ana haki na hukumu, hafanani na miungu,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Mungu mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira,
Kwa watu wote ni mwema, hata wanaomkera,
Amejivika adhama, mche akupe busara,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Mawazoye ni mafumbo, yasoweza fumbuliwa,
Ni azizi yake mambo, kucha kuchwa husifiwa,
Pasi na kuwa na fimbo, hulinda wanoonewa,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Wahadahu la sharika, milele huhimidiwa,
Mbinguni na malaika, duniani na watawa,
Ni nani kama Rabuka, sitara yao makiwa?
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Hapendezwi na sadaka, huupenda utiifu,
Roho iliyovunjika, haidharau Latifu,
Ambaye yuko katika, Utatu Mtakatifu,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Kinywani mwake hutoka, ujuzi na ufahamu,
Hekima huitamka, na kumpa mwanadamu,
Mola mwenye mamlaka, fadhilize si adimu,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Alinitoa gizani, kaniponya na hilaki,
Kanirejesha fajani, Muweza wa mahuluki,
Nisijerudi dhambini, ikawa ndo itifaki,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Duniani nilitanga, nikizengea baraka,
Sikuona la muanga, mtima ukadhurika,
Sasa nimetia nanga, kwa Kahari sitotoka,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Kila siku najihimu, namwendea kwa imani,
Namsujudu Rahimu, narudisha shukurani,
Dua jambo mahashumu, pia ni yenye thamani,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Kaditama kukweleza, yanomhusu Karimu,
Hapa basi nanyamaza, ninaibwaga kalamu,
Nilonena pulikiza, utazidisha elimu,
Nimepiga baragumu, umejuzwa ulimwengu.


Ulipo Njoo Mwandani

Muhibu mtarajiwa, kwani u wapi jamani?
Nakukosa ewe njiwa, hali yangu taabani,
Upweke wanizuzuwa, zimenizidi huzuni,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.

Mahabubu ndiwe dawa, tulizo langu moyoni,
Nina nyonda maridhawa, zilojaa mtimani,
Laiti ningalijuwa, huko uliko nyumbani,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.

Adamu kapewa Hawa, kakufichapi Manani?
Waniandama ukiwa, macho vizuri sioni,
Ningekuwa na mabawa, singekuwa ugonjwani,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.

Mwili wangu waniwawa, asubuhi na jioni,
Majonzini nimetiwa, sina wa kuniauni,
Mimi nitafanikiwa, kinijia maishani,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.

Maisha ya utauwa, nayaishi duniani,
Sitendi yaso muruwa, nimeapa sitazini,
Kukungoja nachachawa, mwengine simtamani,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.

Nataka kukumbatiwa, hapo kwako kifuani,
Mno nitafadhiliwa, kinilaza maziwani,
Hilo nikijaaliwa, tamsifu Rahamani,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.

Toka ulositiriwa, ndo nikutie machoni,
Nikome kuvunjikiwa, raha nipate rohoni,
Naomba utafikiwa, na huu wangu uneni,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani. 
 

Mwenzenu Nimeemewa


Wazo hili nakutubu, Mola litakabalie,

Zangu dhambi ninatubu, naomba radhi nijalie,
Manani nipe jawabu, moyo wangu utulie,
Ipo yoyote sababu, posho usinitilie?

Nielewe e Muhibu, si eti sina imani,

Liniumba na sababu, najuwa hino yakini,
Na hali uko karibu, kwa nini nina huzuni,
Niepushie dharubu, nisifu zako hisani.

Tangu kumaliza shule, kwingi nimesaka kazi,

Nikenda huku na kule, vyeti nikatoa wazi,
Nipate faida zile, wengi wanazomaizi,
Wadai wajiri wale, u haba wangu ujuzi.

Napata ahadi tele, toka kwa wanasiasa,

Wajinadi kwa upole, wasema muda ni sasa,
Tuwache mambo ya kale, tufumbate ya kisasa,
Kwani tutasonga mbele, zikwishe dhiki kabisa.

Tupu zao zote hoja, huwezi kutekeleza,

Mali zetu wamefuja, juu yetu wajitawaza,
Kazi milioni moja, kwa vijana watangaza,
Kughilibu siwe hja, komeni kutupumbaza.


Mausia kwa Wakenya


Yasikilizeni haya, ninyi wanakenya wote,
Tuwacheni nia mbaya, amani idumu kote.
Tutapoeneza maya, utalegezwa upote,
Tazua mbovu tabiya, nchi itakwenda tete.

Obama ametusihi, wakenya tumakinike,
Jirani tusikebehi, moyoni wakubalike,
Tujaliyo maslahi, waume kwa wanawake,
Twendapo tuwasabahi, muradi wasikereke.

Ni nyingi sifaze Kenya, ashukuriwe Rahimu,
Ja risasi zimepenya, duniani zinadumu,
Utalii umefanya, wazuru wataalamu,
Kwa hivyo nawaonya, enyi wasasi haramu.

Uchaguzi ufikapo, tuchague kwa busara,
Tusifuate upepo, tusijepata hasara,
Na watoto wa vikopo, tusiwapigie kura,
Wao mithili ya popo, tahadhari zao sera.

Kusema mengi siwezi, napisha yenu maoni,
Hizi zangu simulizi, zitiliwe maanani,
Sikizeni wasikizi, nilonena kumbukeni,
Mtaongezwa ujuzi, ukwishe umaskini.





1 comment: