Wednesday, 22 May 2013

Jeshurun's Mind: Kiswahili na Mashairi

Baragumu Inalia, Ulimwengu Pulikiza

 

Bismila nakadimu, jinale Muumba wangu,
Tangu abadi hudumu, mfanya nchi na mbingu,
Ana haki na hukumu, hafanani na miungu,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Mungu mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira,
Kwa watu wote ni mwema, hata wanaomkera,
Amejivika adhama, mche akupe busara,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Mawazoye ni mafumbo, yasoweza fumbuliwa,
Ni azizi yake mambo, kucha kuchwa husifiwa,
Pasi na kuwa na fimbo, hulinda wanoonewa,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Wahadahu la sharika, milele huhimidiwa,
Mbinguni na malaika, duniani na watawa,
Ni nani kama Rabuka, sitara yao makiwa?
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Hapendezwi na sadaka, huupenda utiifu,
Roho iliyovunjika, haidharau Latifu,
Ambaye yuko katika, Utatu Mtakatifu,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Kinywani mwake hutoka, ujuzi na ufahamu,
Hekima huitamka, na kumpa mwanadamu,
Mola mwenye mamlaka, fadhilize si adimu,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Alinitoa gizani, kaniponya na hilaki,
Kanirejesha fajani, Muweza wa mahuluki,
Nisijerudi dhambini, ikawa ndo itifaki,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Duniani nilitanga, nikizengea baraka,
Sikuona la muanga, mtima ukadhurika,
Sasa nimetia nanga, kwa Kahari sitotoka,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Kila siku najihimu, namwendea kwa imani,
Namsujudu Rahimu, narudisha shukurani,
Dua jambo mahashumu, pia ni yenye thamani,
Ninapiga baragumu, naujuza ulimwengu.

Kaditama kukweleza, yanomhusu Karimu,
Hapa basi nanyamaza, ninaibwaga kalamu,
Nilonena pulikiza, utazidisha elimu,
Nimepiga baragumu, umejuzwa ulimwengu.

No comments:

Post a Comment