Sunday, 12 May 2013

Jeshurun's Mind: Kiswahili na Mashairi

Ulipo Njoo Mwandani

Muhibu mtarajiwa, kwani u wapi jamani?
Nakukosa ewe njiwa, hali yangu taabani,
Upweke wanizuzuwa, zimenizidi huzuni,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.

Mahabubu ndiwe dawa, tulizo langu moyoni,
Nina nyonda maridhawa, zilojaa mtimani,
Laiti ningalijuwa, huko uliko nyumbani,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.

Adamu kapewa Hawa, kakufichapi Manani?
Waniandama ukiwa, macho vizuri sioni,
Ningekuwa na mabawa, ningetoka ugonjwani,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.

Mwili wangu waniwawa, asubuhi na jioni,
Majonzini nimetiwa, sina wa kuniauni,
Mimi nitafanikiwa, kinijia maishani,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.

Maisha ya utauwa, nayaishi duniani,
Sitendi yaso muruwa, nimeapa sitazini,
Kukungoja nachachawa, mwengine simtamani,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.

Nataka kukumbatiwa, hapo kwako kifuani,
Mno nitafadhiliwa, kinilaza maziwani,
Hilo nikijaaliwa, tamsifu Rahamani,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.

Toka ulositiriwa, ndo nikutie machoni,
Nikome kuvunjikiwa, raha nipate rohoni,
Naomba utafikiwa, na huu wangu uneni,
Ni kama aliyefiwa, ulipo njoo mwandani.  

No comments:

Post a Comment