Ufasaha Hudumani
1. Mola usiyeshabihi, Mwenyezi twakuhimidi,
Twakutukuza Ilahi, madhali hivyo yabidi,
Kwa neema tumewahi, kuwa wako mashahidi,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.
2. Jumanne ndio siku, tulipofika Karura,
Zikatujaza shauku, za uongozini sera,
Sera ziso za udaku, zisizoleta hasara,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.
3. Siku iliyofuata, ndiyo hiyo Jumatano,
Vijana tulitakata, likaanza kongamano,
Sote tulifanya kwata, gwaride liso mfano,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.
4. Mambo mengi ya thamani, tumefundishwa vijana,
Uadilifu kazini, ni nguzo muhimu sana,
Hususa uongozini, ili kuwepo kufana,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.
5. Hayawani kama twiga, ngamia mchwa na tai,
Wanayavalia njuga, mambo yote ya uhai,
Tunapaswa kuwaiga, kuwabeza haifai,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.
6. Ewe mchungaji Juma, mgeni mheshimiwa,
Akurehemu Karima, upate kufanikiwa,
Ujazwe nayo hekima, uzidi kuinuliwa,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.
7. Ulifundisha wanyama, wanayo mafunzo tele,
Kwamba tukiwaandama, sote tutasonga mbele,
Kititi tutasimama, tuishi hata milele,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.
8. Mchungaji Okioma, Yehova akubariki,
Kwa kututendea mema, kutupa kile na hiki,
Mambo yote ulosema, kwayo tutajihakiki,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.
9. Kuwasahau siwezi, wachungaji wengineo,
Mlokuwa hapa juzi, siku zote hata leo,
Awafadhili Mwenyezi, na wote waaminio,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.
10. Nanyi vijana wenzangu, sikizeni kwa makini,
Matamu pia machungu, mtapata maishani,
Ngome yenu iwe Mungu, yeye mtumainini,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.
11. Kituoni nimefika, nawaaga kwaherini,
Kutamka nimechoka, napisha yenu maoni,
Yesu yuaja kumbuka, hilo tujue yakini,
Ufasaha hudumani, Manani utujalie.
No comments:
Post a Comment