Mahojiano kati ya Freddy Macha na Profesa Said Ahmed Mohammed, Mwandishi wa zaidi ya vitabu 30 vya Kiswahili.
Sehemu ya Pili
Kwa wasomaji wapya. Mwandishi Said A Mohammed keshaandika zaidi ya vitabu thelathini ikiwemo michezo ya kuigiza (tamthiliya), riwaya, mashairi na vitabu ya watoto. Riwaya yake maarufu, Asali Chungu, ilichapwa mara ya kwanza, 1976. Mwandishi aliyetopea, Adam Shafi, aliwahi kusema katika mahojiano na mhadhiri wa Kiswahili Ujerumani, Lutz Diegner, kwamba Asali Chungu ni miongoni mwa hazina kuu za Kiswahili na hupenda sana, kukisoma... Endelea...
Freddy Macha
Riwaya zako
tatu zimepishana miaka 36. Je kwanini, muda mrefu toka Utengano hadi Nyuso?
Asali Chungu (1977), Utengano(1980) na Nyuso za Mwanamke (2010), Mhanga Nafsi
Yangu (2012). Vile vile dhamira kuu inamwangalia mwanamke kwa macho na hisia za
kumtetea. Mwandishi mwingine Mwafrika anayesimama upande wa kina mama (hasa
vitabu vyake vya mwanzo) ni Msomali - Nuruddin Farah. Je, kwanini wanaume
muwatetee wanawake? Kwani hawawezi kuandika wenyewe?
Mwandishi Said A Mohammmed
Kuandika riwaya au kazi yoyote ya fasihi kunahitaji wakati,
utulivu na wiitisho wa ndani wa nafsi ya mwandishi. Huwezi tu kujilazimisha
kufululiza. Kisha nadhani vita vya wanawake ni vita vya wanaume pia kama ilivyo
kwamba vita vya wanaume ni vita vya wanawake. Kwa hali hii hakuna suala la kwa
nini? Kwa bahati mbaya waandishi wanaume wachache tu ndio wenye msimamo wa
ukombozi wa wanawake katika fasihi ya Kiswahili. Ama suala la wanawake
kutoandika wenyewe wapo wachache katika fasihi ya Kiswahili wanaoandika hata
kwamba hawajitetei. Jambo hili linashikamana na historia ya wanawake katika
jamii zetu. Wanawake popote pale wamekuwa katika historia ya ukandamizwaji, je
kwa nini tusiwatetee?.
Freddy Macha
Sauti unayotumia kuelezea kisa chako
katika Nyuso za Mwanamke ni tofauti na Utengano na Asali Chungu. Mtindo wa
Nyuso ni wa “ki-maelezo” zaidi kuliko kutumia wahusika kama Semeni, Zuberi na
Dude (Asali Chungu) na Maimuna, Maksudi na Shoka (Utengano). Je kwanini ukaamua
kufanya hivyo?
Wachapishaji wake mwanafasihi Said
Mohammed wenye makao makuu Nairobi na ofisi mbalimbali Afrika Mashariki.
Mwandishi
Said A Mohammed
Kila kazi ya fasihi katika utanzu wake ni kama mtoto ambaye
amezaliwa na mama na babake. Hawezi mtoto mmoja awe sawa na mtoto mwengine wa
tumbo moja. Huu ni ukweli pia katika uandishi wa kubuni. Lakini sidhani kwamba
simulizi yangu katika Nyuso za Mwanamke ni simulizi ya kueleza tu, yaani
“telling or descriptive”, bali kwa sehemu kubwa ni ya kuonyesha “showing”
kupitia wahausika wangu. Na kwa upande mwingine haiwezakani riwaya kuisimulia
kwa mtindo mmoja bali kwa mshikamano wa mitindo miwili.
Freddy Macha
“Nyuso..” imechukua
muda mrefu sana kumshika msomaji kuliko vile visa vya mwanzo.Hadi ukurasa wa 44
ndipo kisa kinapoanza kujitokeza kwamba chamhusu mtu na mzazi wake. Mwandishi
ana uhuru wa kuchagua mtindo wa kuelezea riwaya yake. Je kwanini ukachagua
mtindo huu wa mafumbo mafumbo na kuchelewesha habari na maudhui? Je kadri
mwandishi unavyoendelea kukomaa unashawishika kufanya majaribio ya ki fani? Na
je, umepata “matokeo” au mrejesho nyuma gani kutoka kwa wasomaji wako kuhusiana
na kisa hiki?
Mwandishi Said A Mohammed
Kama kweli wasomaji wote
wanahisi kuchelewa kwa hadithi ya Nyuso za si hakika. Labda inaweza kuwa riwaya
hii ina katika matapo (layers) mengi. Isitoshe, mhusika mkuu Nana ana tatizo la
kuzungumza ndani ya nafsi yake na kuzungumza mwenyewe kwa mwenyewe, kwa hivyo
mwanzo hakuna mgongano wa wahusika ambao unatazamiwa kumchangamsha msomaji.
Nana ana tatizo linalomfanya aelezee yeye nani na kwa nini ametengana na mamake,
jambo ambalo ni msingi mkubwa wa hadithi hii. Lakini hata magwiji wa riwaya
wanazungumziwa kuwepo “purple colours” na uchangamfu katika kazi zao – yote
mawili.
Freddy Macha
“Utengano” na “Nyuso” zina
mlolongo wa maneno mapya au “magumu” ya Kiswahili. Huu ni mtindo mzuri sana wa
kuendeleza lugha yetu.Si waandishi wengi wanaotupa “sherehe” kama hii. Labda
tutegemee kwamba “Asali” ikichapishwa tena pia iwekewe “sherehe” , maana ina
maneno mengi “magumu”?
Mwandishi Said A Mohammed
Kwanza niseme
kwamba Kiswahili kina utajiri mwingi lakini waandishi wachache wanasahau hivyo
au hawataki kusikia wenzao wanavyosema na wanavyoandika. Pili, wazo lako
nalikubali kwa ukamilifu.
Freddy Macha
Visa vyako huchimba undani
wa wahusika kuonyesha maisha magumu lakini hapo hapo kutekenya ndoto njema na
fikra za wanadamu. Ukurasa 118 (Asali) tunaonyeshwa Dude alipopata ahueni baada
ya kufarijiwa na mke wa Zuberi. Mwandishi unasema: “Ata! Dude hataki tena kufa;
anataka aishi.Ni nani asiyetaka kuishi?” Utengano hali kadhalika.Bi Kocho
anaonyesha ari ya kike akiongea na Farashuu (uk 61): “Sifi kwa ufukara, nikafa
kwa kuteswa na mtu. Wakati wa kuogopa umekwisha. Hata kama Maksuudi angalikuwa
Mzungu.” Na “Nyuso” hali kadhalika (uk 39): “Nilihisi kwamba haki ya kuwa huru
ni haki yangu ya kwanza ya msingi.” Je, lengo na msimamo wako mwandishi
kuonyesha jazba ya wanadamu na kwamba ushindi ni kheri yetu kuliko fikra za
kushindwa na kukata tamaa na maisha? Au imetokea tu?
Mwandishi Said A
Mohammed
Unajua kutaka tusitake, kila mwandishi ana msimamo na falsafa
yake. Mimi siwezi kuwafanya wahusika wangu wakate tamaa. Bila ya tamaa binadamu
hawezi kujikomboa. Ukweli ni kwamba bado tunatawaliwa na tena vibaya vibaya.
Freddy Macha
Riwaya hizi tatu zimeelezewa ndani
ya maisha ya Visiwani peke yake. Lakini mwandishi umetembea na kuishi mazingira
mengine mfano Kenya, Tanzania Bara na Ulaya. Kwanini huangalii huko pia kama
ulivyofanya katika hadithi yako fupi “Tazamana Na Mauti” (Damu Nyeusi)
inayoangalia maisha ya London?
Mwandishi Said A Mohammed
Hadithi mara nyingi huja na kuendana na
mandhari (setting) yake. Baada ya kukaa nje ya Zanzibar na Tanzania nimepata
uzoefu wa nje, kwa hivyo soma kazi kama Baba Alipofufuka, Dunia Yao, Mhanga
Nafsi Yangu n.k, utaona kwamba nimefaidikia kimaudhui na kimandhari
yanayokamatana katika uwili mmoja. Si kazi zangu zote ni za nyumabani tu.
Freddy Macha
Kifani
una lugha ya kipekee inayochora mandhari, wahusika, hisia, mazingira. Mifano
iko mingi sana – ila tuchague michache ndani ya “Utengano” na “Asali”
zinavyochambua mazingira ya maskini- kilabuni (Utengano, uk 138-143 ) ambapo
wanawake wawili – Maimuna na Kijakazi wanavyogombana. Hapa umeshika taji la
kukionyesha Kiswahili kilivyo kitamu: “Kijakazi mwenye tabia ya uso wa samaki
usiosikia viungo”; “Shoka alitia pamba masikioni”; “Nani anayeshtua watu akitupiwa
mbwa hamtaki”; “Kijakazi alijitazama akajiona kapwaya kweli”; “Alikua shetani
na aliweza kummeza yeyote.” Na kadhalika. “Asali Chungu,” inayachora maisha ya
wananchi kwa undani. Kama wakati Semeni akijipamba. Uk 42 : “Baadaye alikunja
miguu yake akaanza kuisinga kwa baki ya mafuta yaliyoroa mikononi mwake.
Akarejesha zana zake chumbani na kurudi kukaa kwenye kiti cha marimba pale pale
kwenye baraza. Alikua kakaa kwenye kile kiti, kinyume mbele, kajivuta nyuma na
kukimwaya kiuno chake upande wa ukutani. Kifua na mikono ikalalia kiegemeo cha
kiti, kichwa chake kimeelemea kwenye mikono yake aliyoipachika pamoja; akawa
anamwangalia Pili aliyejitia hajamwona, anamfundika kijakazi mkia wa mwisho.”
Je, una nini la kuwafundisha waandishi wachanga wanaokua sasa hivi namna ya
kuyasifia na kuyapamba na kuyachora vizuri mazingira wanayoyaandika. Waandishi
wengi vijana leo wanaandika michezo ya sinema, wanaandika tenzi za rapu (Bongo
Flava) wanaandika hadithi fupi fupi. Ila mara nyingi hawajaonyesha mazingira kitaswira.
Nini siri wanayoikosa? Ukiacha kipaji yaani.
Mwandishi Said A Mohammed
Kwanza wakipende Kiswahili, pili, wakisikilize na tatu wakisome kutokana na
wale wanaokipenda Kiswahili. Wakubali kuiga, maana wigo si mbaya iwapo
utatumika kwa kufunguka tu.
Freddy Macha
Tuangalia mambo mawili pia yanayohusu lugha.
Kwanza tueleze vipi ukaunda misemo mizito kwa maneno machache. Yanatoka wapi?
Mfano: Nyuso (Sura 7; uk 70); “Maiti kasoro nukta.” Asali (Sura 11; uk 143) :
“Ulimwengu ni mchafu. Je, yeye mlimwengu awe vipi?” Asali (Sura 8; uk 101)
“Mungu haombwi; hutoa.” Utengano (Sura 10; uk 118 ) : “Bora nusu ya shari
kuliko shari kamili.” Pili, tusaidie tafsiri ya maneno na misemo ya visiwani
ambayo haieleweki kwa baadhi ya wasomaji wa bara: “Sherehe za wana
kindakindaki” (Asali, Sura 12; uk 159) “Kuruka adi-mfundo” (Asali, Sura 8; uk
111) Je ni “andasa” au “andis”? (Asali, Sura 4; uk 50) “Hapendi, hataki, hajali
wala habali” – (Utengano, Sura 1; uk3) “Mkareti” (Utengano, Sura 2; uk 20)
Mwandishi
Said A Mohammed
Nafikiri misemo na maneno hayo hapo juu yanatokana na upeo
wangu wa kubuni na ukwasi wa lugha nilioupata katika utamaduni wangu. Ndio ule
utamu wa lugha ulioutaja hapo juu. Mwandishi lazima awe mweledi na mwepese wa
kutumia maneno na misemo yenye kuvutia na kushangaza. Mbali na hayo mwandishi
lazima asikilize watu wanavyosema katika jamii husika na utamaduni wake unaotoa
nafasi ya kuunda misemo na kauli za mvutio. Kindakindaki ni mtoto wa mtu mkubwa
kama vile mfalme. Adimfundo ni aina ya mchezo wa kuruka vyumba vilivyochorwa
ardhini. Neno andasa ni nomino na andis(i) ni kitenzi. Hapendi, hataki, hajali
wala habali ni kauli ya msisitizo wa kutopenda. Mkareti ni aina ya mmea wenye
mbegu ngumu kama mawe na pia unazungukwa na miba.
Profesa Said A Mohammed, alistahafu
kazi ya kufundisha Kiswahili vyuo vikuu mbalimbali duniani, mwaka jana.
No comments:
Post a Comment